Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi amesema Jeshi la Polisi Mkoani humo limekamata mawe yenye madini ya dhahabu yenye uzito wa gramu 6753.4 na thamani ya shilingi bilioni 9.2 yakitoroshwa kutoka kwenye mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu wilayani Kahama huku pia likikamata Carbon yenye mchanga wenye madini yanayodhaniwa kuwa ni dhahabu yenye uzito wa Kg 261 ambayo thamani yake bado haijajulikana katika maeneo ya Manzese Kahama.
ACP Janeth Magomi ameyasema hayo mbele ya vyombo vya habari leo Jumatano Agosti 23,2023 kuwa mali hizo zimekamatwa kwa kipindi cha kuanzia julai 26 hadi Augusti 22 baada ya kufanya misako na doria katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Shinyanga.
“Pia tumekamata jumla ya lita 603 za mafuta aina ya Diesel katika maeneo tofauti ya mradi wa Reli ya mwendokasi SGR. Mafuta haya yamewekwa kwenye chupa ndogo, wezi wa mafuta sasa hivi wamebuni mbinu ya kutumia vichupa badala ya madumu makubwa”, amesema Kamanda Magomi.
Amesema , katika misako hiyo Jeshi la polisi Shinyanga pia limefanikiwa kukamata Bunduki aina ya Riffle yenye namba 2/49PF78701 ambayo ilikuwa inatumika katika shughuli za ulinzi bila kibali.
Vitu vingine vilivyokamatwa na jeshi la polisi ni dawa za kulevya aina ya Bangi yenye uzito wa Kg 71, seti moja ya computer, Pikipiki 03, tiles Box 14, mabomba 06 ya chuma na vipande 09, Mabati 17, Plastic 3 za rangi ya majumba, mifuko 02 ya Cement, mifuko 7 ya chokaa, pamoja na Pakti 120 za vipodozi vinavyoaminika kuwa na sumu.
Kamanda Magomi amesema, jumla ya watuhumiwa 31 wanashikiliwa katika vituo mbalimbali vya Polisi kuhusiana na makosa hayo na wengine wamepewa dhamana huku wakisubiri kufikishwa mahakamani.
#KonceptTVUpdates