Ukisikia kulipa fadhila ndiko huku ambapo Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa hii leo Augosti 31, 2023 limepokea msaada wa gari moja aina ya Toyota Premio na pikipiki moja aina ya Boxer.
Msaada huo umetolewa na kampuni ya Mufindi Wood Poles Plant and Timber Ltd ya wilayani Mufindi iliyotoa gari hiyo na kampuni ya Udzungwa Corridor ya wilayani Kilolo iliyotoa pikipiki huku lengo likiwa ni kuimarisha doria na kupambana na uhalifu.
Akizungumza na wanahabari leo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, ACP Allan Bukumbi amesema vitendea kazi hivyo vimepatikana kutokana na ushirikiano mzuri uliopo baina ya Jeshi la Polisi na wadau mbalimbali wa maendeleo.
Pamoja na msaada huo alisema jeshi la Polisi limefanya matengenezo ya magari 12 yaliyofanyiwa ukarabati wa jumla na kupakwa rangi upya.
ACP Bukumbi amesema zaidi ya Sh Milioni 28.6 zilizopatikana kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali ikiwemo kampuni ya Asas Group, Ivory na Toyota Tanzania Ltd zimetumika katika matengenezo hayo.
Alisema magari hayo yatatumika katika kuzuia na kupambana na uhalifu ikiwemo udhibiti wa doria za barabarani ili kuzuia ajali zinazosababishwa na madereva wasiotii sheria.
#KonceptTVUpdates