Umoja wa Afrika umeisimamisha Niger katika shughuli zake zote kufuatia mapinduzi ya kijeshi ya yaliyofanyika mwishoni mwa mwezi uliopita na kurejelea wito wake kwa viongozi wa kijeshi kumwachia Rais aliyepinduliwa Mohamed Bazoum.
Aidha, Umoja wa Afrika umerejelea wito wake kwa viongozi wa kijeshi kumwachia mara moja rais aliyepinduliwa Mohamed Bazoum ambaye anazuiliwa tangu mapinduzi na kuwataka wanajeshi hao kurejea kwenye makambi yao.
Hata hivyo viongozi wa kijeshi wamekataa shinikizo la kuachia madaraka na kupendekeza kipindi cha mpito cha miaka mitatu ili kuandaa uchaguzi, mpango uliokataliwa na ECOWAS.
Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika, limesema katika taarifa yake kwamba limefahamu maamuzi ya Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi ECOWAS ya kupeleka kikosi cha dharura nchini Niger, lakini limeitaka tume ya Umoja wa Afrika kutathmini athari za kiuchumi, kijamii na kiusalama za uingiliaji kati kijeshi.
Maazimio hayo yaliyosomwa katika tamko la Jumanne yalipitishwa na baraza lililoketi Agosti 14. Jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi ECOWAS, tayari ilishaanzisha vikwazo dhidi ya Niger, vilivyoidhinishwa na Umoja wa Afrika.
ECOWAS ilisema kuwa iko tayari kuwatuma wanajeshi nchini Niger, endapo juhudi za kidiplomasia zitashindikana. Umoja wa Afrika umetoa wito kwa wanachama wake wote na jumuiya ya kimataifa kujizuia na hatua yoyote inayoweza kuhalalisha utawala wa kijeshi wa Niger.
Na wakati huohuo umekataa vikali uingiliaji wowote wa nje katika mzozo huo unaofanywa na mtu au nchi yoyote nje ya Afrika, ikiwa ni pamoja na ushirikiano na makampuni ya kijeshi ya kibinafsi, wito unaoonekana kulilenga kundi la mamluki la Urusi Wagner, ambalo linafanya kazi katika nchi jirani ya Mali.
#KonceptTVUpdates