Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amebainisha kuwa Tanzania itaendelea kuunga mkono jitihada za agenda ya chakula na lishe kwa kuendelea kupewa kipaumbele kwa nchi wanachama wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika.
Waziri Ummy amebainisha hayo leo Agosti 30, 2023 wakati akiendelea kushiriki kikao cha 73 cha Mawaziri wa Afya wa nchi wanachama wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika chenye lengo la kujadili masuala mbalimbali katika Sekta ya Afya.
“Tanzania ni miongoni mwa nchi wanachama wa Shirika la Afya Duniani kanda ya Afrika hivyo tutaendelea kupambana na tatizo la upungufu wa chakula na lishe bora inayopelekea ukondefu (Malnutrition)”, amesema Waziri Ummy
Mawaziri wa Afya wa Nchi wanachama wa WHO Kanda ya Afrika wakati wakiendelea kuchangia mada katika kikao hicho wamesema sababu zinazopelekea kupungua kwa uzalishaji wa chakula ni pamoja na mabadiliko ya tabia nchi, vita vya wenyewe kwa wenyewe, changamoto zilizotokana na ugonjwa wa COVID-19, ukame na mafuriko.
Pia, wamesema nchi za Afrika zimeonesha ongezeko la matatizo yatokanayo na ukosefu wa lishe ni pamoja na kutozingatia ulaji sahihi wa vyakula (Balanced diet).
Kwa upande wa wadau pamoja na mashirika ya Kimataifa yanayojishughulisha na masuala ya chakula na lishe wakiwemo UNICEF, FAO, Sun MOVEMENT, AFRICAN UNION, Nutrition International na wengine wameahidi kuendelea kusaidia kuchangia na kushirikiana na Serikali za Afrika kwa lengo la kupunguza changamoto zitokanazo na lishe.
#KonceptTVUpdates