Serikali kupitia Wizara ya Afya imelishukuru Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa namna lilivyoshirikiana na Tanzania wakati wa kudhibiti janga la ugonjwa wa Marburg na kupelekea ugonjwa huo kudhibitiwa kwa haraka sana na hivyo kuzuia kusambaa maeneo mengine
Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe wakati akichangia mada kwa niaba ya Waziri wa Afya katika mkutano wa WHO kanda ya Afrika huko Gaborone nchini Botswana.
Aidha, Dkt. Magembe ameelezea mafanikio yaliyopatikana katika kuimarisha huduma za afya kuanzia ngazi ya Msingi na kupelekekea kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi, vifo kwa Watoto chini ya miaka mitano. Pia kuiwezesha Tanzania kuwa kati ya nchi tano za mwanzo ambazo zimeweza kufikia malengo ya 95 95 95 ya mapambano dhidi ya UKIMWI.
“Kwa sasa asilimia 96 ya wanaokadiriwa kuishi na VVU wamepima na kutambua hali zao za maambukizi. Kati ya hao asilimia 98 wanatumia dawa za kufubaza VVU na kati ya hao asilima 97 wamefikia kiwango cha kufubaza VVU”. Amesema Dkt. Magembe.
Kutokana na ongezeko la magonjwa ya mlipuko na madhara mengine ya kiafya ikiwemo dharura mbalimbali duniani, Dkt. Magembe amesisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kuwezeshwa kukabiliana na majanga hayo kwa kuimarisha mifumo ya Afya itakayowezesha kuzuia, kutambua mapema na kukabiliana na majanga hayo kuanzia ngazi ya Jamii.
#KonceptTVUpdates