Nchi ya Tunisia na Libya zimetangaza makubaliano ya kushirikiana na wajibu wa kutoa hifadhi kwa mamia ya wahamiaji ambao wamekwama mpakani, huku wengi wao wakiwa wamekwama kwa zaidi ya mwezi mmoja.
Mashirika ya misaada yanasema makundi matatu ya takriban wahamiaji 300 kutoka nchi za Afrika chini ya jangwa la Sahara kwa ujumla walikwama huko na kuishi katika hali ya kutishia maisha yao.
Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani ya Tunisia, Faker Bouzghaya anasema kuwa wakati wa kikao cha pamoja na maafisa wa Libya mjini Tunis, wamekubaliana kushirikiana na makundi hayo ya wahamiaji ambao wako mpakani. Pia anasema Tunisia itachukua jukumu la kundi la wanaume 76, wanawake 42 na watoto 4.
Faker anasema makundi hayo yalihamishwa siku ya Jumatano na kupelekwa kwenye vituo katika miji ya Tatouine na Medenine na kupatiwa huduma za afya na kisaikolojia, kwa msaada wa shirika la Mwezi Mwekundu la Tunisia.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Libya itachukua kundi lililobaki la wahamiaji kati ya 150 na 200. Wizara ya mambo ya ndani ya Libya mapema Alhamisi ilitangaza kufikiwa kwa mkataba wa pande hizo mbili wa kumaliza mzozo wa wahamiaji wasio wa kawaida waliokwama kwenye eneo la mpakani.
Katika taarifa yake baadaye, ilisema kulikuwa hakuna wahamiaji zaidi waliokwama kwenye mpaka kufuatia makubaliano hayo, ikiongezea kwamba doria za pamoja zimeandaliwa ili kulilinda eneo la mpakani.
Mivutano ya rangi imeongezeka nchini Tunisia katika mji wa Sfax baada ya mauaji ya Julai 3 ya mwanamme mmoja raia wa Tunisia kufuatia ugomvi na wahamiaji. Takribani Waafrika weusi 1,200 waliondolewa kwa nguvu na majeshi ya usalama ya Tunisia, na kupelekea kwenye mikoa ya jangwani kwenye mpaka na Libya na Algeria, Human Rights inasema.
Shirika la Mwezi Mwekundu Tunisia Julai 12 liliwapatia makazi kiasi cha wahamiaji 630 waliogundulika huko Ras Jedir, pamoja na wengine 200 ambao walisukumwa kuelekea Algeria.
Kwa mujibu wa kituo cha VOA Swahili, waandishi wa habari wa AFP na vyombo vingine vya habari waliripoti kwamba kiasi cha wahamiaji 350 bado wamekwama huko Ras Jedir katika wiki zilizofuata.
Takribani kilometa 40 kusini mwa Al Assah, mamia ya wahamiaji wengine walionekana kumiminika kuingia nchini Libya, huku wakiwa hawana fursa ya chakula, maji na wala mahitaji muhimu mpaka walipookolewa na walinzi wa mpakani wa Libya mapema mwezi Agosti.
Tangu mwezi Julai, takribani wahamiaji 27 wamegundulika kufariki baada ya kuachwa katika eneo la mpakani kati ya Tunisia na Libya na wengine 73 hawajulikani walipo. Pia mpaka siku ya Jumatano wahamiaji waliendelea kuwasili nchini Libya huko Al Assah kwa kiwango cha takribani watu 50 kwa siku kabla ya kuokolewa na walinzi wa Libya.
Nchi hizo mbili za Afrika Kaskazini ni njia kuu kwa wahamiaji na waomba hifadhi wanaojaribu kufanya safari hatari kwa kutumia boti chakavu kwa matumaini ya kutafuta maisha bora huko Ulaya.
#KonceptTvUpdates
#AFP