Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hashimu Komba amewekea mkakati wa kufanya usafi kwa kuboresha mazingira katika maeneo ya umma Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo kutia ndani madaraja, makutano ya barabarani, vivuko na stendi ya Magufuli.
Ameyasema hayo jumatatu Agosti 21 mbele ya waandishi wa habari kuhusu ufunguzi wa kampeni ya mazingira wilayani humo unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu yenye kaulimbiu ‘Kataa uchafu, safisha, pendezesha Ubungo’.
Amesema uboreshaji huo unahusu upandaji wa bustani kwa ajili ya mapumziko ya watu na huduma ya intaneti bure na inatarajiwa kuzinduliwa rasmi jumamosi hii ya Agosti 26 eneo la Manzense.
Komba amesema lengo la kampeni hiyo ni kudhibiti taka ngumu kwenye Kata zote 14 mitaa 90, ili jamii ijenge utamaduni wa kutunza mazingira na kuifanya Ubungo kuwa kivutio.
“Kampeni hii itakuwa inatoa zawadi ya pikipiki, katika mitaa 90 mtaa ambao utaonekana umefanya vizuri kuliko mitaa yote utakabidhiwa pikipiki mbili.
“Pikipiki ya kwanza itakuwa ni ya Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa na pikipiki ya pili itakuwa ni mali ya mtaa ambayo itakuwa imesajiliwa kwa namba za halmashauri.”
“Mtaa wa kwanza ambao utafanya vizuri tutawakabidhi shilingi laki sita, mtaa wa pili utakabidhiwa shilingi laki tatu na mtaa wa tatu shilingi laki mbili,” amesema Komba.
Hata hivyo mkuu huyo wa wilaya ya Ubungo Komba amesema kwa mitaa ambayo itafanya vibaya Zaidi kuna zawadi yao ambayo utapewa bendera yenye maneno “Balozi wa Uchafu,” mpaka pale utakapojirekebisha.
#KonceptTVUpdates