Umoja wa Watanzania waliosoma nchi mbalimbali (JATA) umeweka mpango mkakati wa kipekee wa kuwafikia wale ambao wametoka katika gereza la Kikururu (Gerazani) kwa kuanzisha miradi ya maendeleo inayolenga kuwajengea uwezo wa kuishi kwa kujipatia kipato.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa JATA, Bw. Gregory Mlay, wakati wa kikao kazi cha wanachama kilichofanyika mjini Morogoro, kwa ushirikiano na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA). Kikao hicho kiliwakutanisha viongozi wa Taifa (EXCOM) na viongozi wa kanda za JATA, na kilijadili masuala mbalimbali ya utekelezaji kwa mwaka 2023/2024 na kuimarisha umoja huo.
Bw. Mlay alieleza kuwa viongozi kutoka Kanda ya Morogoro, Pwani, Kaskazini, Kusini, Iringa, Kanda ya Ziwa, Kati, na Kanda ya Zanzibar walishiriki kikao hicho. Alisema kuwa katika mwaka huu, umoja huo umeamua kutekeleza miradi sita iliyopitishwa katika mkutano mkuu wa mwaka uliopita (2022), ikiwemo mpango mkakati wa kuwafikia waliotoka gerazani kwa kuwajengea uwezo wa kuishi kwa kuanzisha miradi ya maendeleo.
Mlay alibainisha kuwa hatua nyingine za utekelezaji ni pamoja na kufuatilia na kuwafikia wanachama wa umoja huo waliopo katika kila kanda. “Mpango mkakati wa kuwajengea uwezo waliotoka gerazani ni sehemu ya jitihada zetu za kuboresha hali ya maisha ya watu na kuongeza ufanisi katika jamii,” alieleza Mlay.
Katibu Msaidizi wa Umoja huo, Bibi Edina Ngelageza, aliongeza kuwa pamoja na miradi hiyo sita, kuna miradi mingine inayotekelezwa na wanachama binafsi ambao wamehitimu katika taaluma mbalimbali kama afya, maji, viwanda, mazingira, elimu, na utawala bora. Ngelageza alibainisha mafanikio ya miradi hiyo, ikiwemo mradi wa usafi wa mazingira unaotekelezwa kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, ambao umesaidia kuboresha utunzaji wa mazingira nchini.
Mwakilishi wa JICA, Bi. Evona Mathew, alieleza kufurahishwa kwao na jitihada za umoja huo na jinsi inavyosaidia katika kubaini matunda ya ufadhili wao katika sekta mbalimbali. “Hii imekuwa ni njia sahihi ya kufuatilia na kubaini matunda ya ufadhili wa JICA unaoutoa katika sekta mbalimbali kwani unaleta tija katika jamii,” alisema Bi. Evona.
#KonceptTvUpdates