Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi,Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu imewezesha vijana 260 kwenda Israel kujifunza na kupata uzoefu katika fani ya kilimo na mifugo kwa kutumia teknolojia ya kisasa. SERIKALI ya Tanzania kwa kushirikiana na Israel wameendelea na jitihada za kukuza ujuzi kwa vijana kwenye sekta ya kilimo, ambapo takribani vijana 260 wanapelekwa nchini Israel kupata mafunzo ya kilimo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, wakati wa hafla ya kuwaaga vijana wanaotarajiwa kwenda nchini Israel kuhudhuria mafunzo ya kilimo cha kisasa, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu), Profesa Jamal Katundu amesema wanafunzi hao watakuwa na mafunzo ya darasani lakini pia mafunzo kwa vitendo na yamegharamiwa kiasi cha Sh.milioni 256 na serikali kupitia Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi inayoratibiwa na ofisi hiyo na kuwaasa vijana hao kutumia vizuri fursa hiyo.
Amesema fursa hiyo imepatilana kutokana na jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu wa Israel ambao wamekuwa wakizungumzia suala hilo kwa ajili ya kujenga uwezo wa vijana kwenye sekta ya kilimo
Naye, Mkurugenzi wa Idara ya Aijra na Ukuzaji Ujuzi wa Ofisi hiyo, Ally Msaki, amesema tangu mwaka 2019 serikali imepeleka vijana kutoka vyuo mbalimbali zaidi ya 700 nchini Israel kwenda kujifunza.
Alisema wanafunzi hao wanapokuwa nchini Israel ni fursa nzuri kwao kwani mbali na kupata mafunzo ya utaalamu wa kisasa, lakini pia wanakua wanafanya kazi na kulipwa.
Prof. Katundu amewasihi vijana hao kuitumia elimu wanayoipata nchini humo, ili waweze kujikwamua kiuchumi na kuwa chachu katika jamii na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Naibu Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam anayeshughulikia mambo ya utafiti Prof. Nelson Boniface amesema fursa hizi zinazotolewa na BBT, ambayo ni mafunzo kwa vitendo yako sawasawa na matakwa ya serikali, ambapo wanataka vijana wapate umahiri pale wanapokuwa wamejifunza darasani waweze kutumia maarifa yao katika kuzalisha.
Pia amesema katika programu hiyo hadi sasa wameshiriki kwa miaka miwili na kwa mwaka huu wanapeleka vijana 32, hivyo kama chuo ushiriki wao unaanza kuchukua kasi kwa kuiunga mkono serikali na kuwa wanufaika katika mradi huo.
#KonceptTVUpdates