WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,Mhe. George Simbachawene ameipongeza Watumishi Housing Investments (WHI) kwa kujenga nyumba za gharama nafuu nchini kwa ajili ya kuwauzia na kuwapangisha watumishi wa umma huku akiwasisitizia kuwauzia watumishi ambao ni vijana na wanaoanza maisha.
Pongezi hizo amezitoa leo Agosti 24,2023 wakati wa ziara yake ya kukagua nyumba 1000 za watumishi wa Umma zilizopo Kisasa na Ndejengwa jijini Dodoma zinazojengwa na Watumishi Housing.
Waziri Simbachawene amesema utekelezaji wa nyumba bora za watumishi huo ni mwelekeo mzuri katika kutekeleza sera ya makazi kwa watumishi wa Umma inayotekelezwa na Serikali ya awamu ya sita lakini pia imeelezwa katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Aidha,Waziri Simbachawene amewapongeza wateja wanaonunua nyumba zinazojengwa na Watumishi Housing ambapo nyingi ni Taasisi za Umma na Watumishi wa Umma.
“Na hapa ndipo ninapotaka nitie msisitizo kwamba watumishi tunawaolenga ni wale wanaoanza kazi ama ambao wameenda katika maeneo ambayo hawana nyumba,”amesema Simbachawene.
Amesema nyumba hizo zisilengwe kuwauzia watumishi kwa sababu ya nafasi zao au ya uwezo wao ilenge kuwashawishi hata wale ambao hawana uwezo wa kujenga nyumba.
Amesema wapo baadhi ya vijana ndio wanaanza kazi badala ya kufikiria kutafuta kiwanja na fundi inakuwa ngumu hivyo nyumba hizi zilenge pia kwa vijana hao.
“Nyumba kama hii inamtosha kabisa kijana anaeanza maisha lakini ukimwambia aanze kutafuta kiwanja na urasimu huko tunapoteza watu wengi elimu ipelekwe hasa kwa watumishi wanaoanza kazi,”amesema Waziri Simbachawene.
Pia amesisitiza kujenga Majengo katikati ya miji ili kuwasaidia wafanyakazi na kuwapunguzi gharama za usafiri.Katika hatua nyingine,Waziri huyo ameagiza wale walionunua nyumba lakini hawajakabidhiwa hati,Shirika hilo wafanye mchakato kuhakikisha walionunua wanapatiwa hati zao.
Vilevile ametaka mikataba ya upangishaji na ununuaji iangaliwe isiwe ya kumkomoa mtumishi. Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete amesema kazi inayofanywa na Watumishi Housing ni nzuri na Serikali inajivunia uwepo wao.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Watumishi Housing Investment (WHI), Dk. Fred Msemwa amesema hadi sasa wameweza kutengeneza nyumba 203 ambazo Waziri na Naibu Waziri wamepata nafasi ya kuziona.
Amesema katika nyumba hizo asilimia 99 zimeishauzwa kwa watumishi wa umma ikiwa na maana nyumba 2 pekee ndizo bado hazijauzwa lakini zinaweza kuuzwa wakati wowote kutoka sasa.
“Mimi nichukue nafasi hii kusema kwamba sisi kama WHI tutaendelea kufanya vizuri huku tukizingatia maelekezo ili utekelezaji wa Mpango wa makazi kwa watumishi wa Umma uende vizuri na watumishi zaidi waweze kunufaika na huduma hiii inayotolewa na Serikali.
“Lengo ni watumishi waweze kufanya kazi katika mazingira bora na salama ambayo yatawahakikishia ufanisi na utulivu katika kuwatumikia watanzania katika sekta mbalimbali ambazo wanazohudumu,”amesema Dkt.Msemwa