Alec Steele ana umri wa miaka 82 na amegunduliwa kuwa na ugonjwa wa maisha, lakini ameazimia kuendelea kucheza kriketi, hata akiwa amefungwa tanki la oksijeni mgongoni.
Alec anaugua idiopathic pulmonary fibrosis – ugonjwa ambao huharibu utendaji wa mapafu na muathiriwa huishi kati ya mwaka mmoja na mitano. Lakini miaka mitatu baada ya kugunduliwa, mchezaji huyo wa zamani wa kimataifa wa Scotland amerejea tena ulingoni.
“Lazima uwe na mtazamo chanya,” anasema. “Nilijiambia, ingawa nimefahamishwa ni ugonjwa maisha, nitajitahidi kadri niwezavyo ili nirudi kucheza kriketi. “Nadhani jambo muhimu zaidi lililonijia ni kutowahi kukata tamaa.” Alec anasema miezi sita ya kwanza ilikuwa ngumu kwake baada ya kuambiwa anachougua kwani ilimuathiri kimwili na kiroho.
Pamoja na utendaji wa mapafu yake kuwa chini ya asolimia 30, kufanya shughuli za kawaida kama vile kuzunguka na kupanda juu ilikuwa ngumu. Lakini alipokuwa akihudhuria kitengo cha huduma shufaa katika Hospitali ya Royal Victoria huko Dundee, aliwafahamisha wafanyakazi kwamba alitaka kujiweka sawa ili kucheza mchezo mmoja wa mwisho.
Kufuatia juhudi ya miezi kadhaa ya kujiimarisha kiafya na kupitia tiba maalum, Alec alifanikisha ndoto yake ya kucheza walau mechi moja huko St Andrews mwaka jana. Anasema: “Nilikuwa na fursa kubwa ya kuingia uwanjani kucheza kriketi kwa mara nyingine.
“Kitu ambacho mchezo huo ulinifunza ni kwamba naweza kudaka mpira na ningeweza kutunza wiketi kidogo.” Tangu mchezo huo wa kwanza, Alec hajaangalia nyuma.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 82 sasa anamaliza msimu wake wa pili akicheza kwa msaada wa tanki lake la oksijeni – na amedhamiria kuwa atakuwa kwenye kisiki msimu ujao pia.
“Nitaponea, farasi-mwitu hawataniweka mbali,” anasema. Alec sasa anamaliza msimu wake wa pili akicheza kwa msaada wa tanki lake la oksijeni. Labda haishangazi kwamba Alec amevunja matarajio yote juu ya kupona kwake na kurejelea mchezo huo.
Huyu ni mtu ambaye alicheza kriketi ya ligi hadi alipokuwa na umri wa miaka 64 katika Klabu ya Kriketi ya Forfarshire. Katika uchezaji wake wa kimataifa, alikipiga katika viwanja maarufu kama Lords na The Oval, akiacha nafasi ya kucheza mchezo wa kaunti nchini Uingereza ili kuzingatia kazi yake nyingine kama mbunifu.
Na anasimulia jinsi alivyofanikiwa kumpiga nguli wa kriketi Viv Richards ili tu mwamuzi aangalie upande mwingine. Lakini wakati kriketi imekuwa sehemu kubwa ya maisha yake, Alec sasa anataka kutumia hali yake kueneza ufahamu kuhusu ugonjwa idiopathic pulmonary fibrosis.
Anasema hajawahi kusikia ugonjwa huo kabla ya apatikane nao, akiuita “ugonjwa wa kutisha”. Imemfanya atumie oksijeni kati ya saa 16 na 24 kwa siku na inaweza kumchukua siku kupona kutokana na mechi. Licha ya hayo, Alec hapendi kuzingatia mapungufu – wazo hasi likiingia akilini mwake yeye hulisukumia mbali.
Katika mechi yake ya kwanza huko St Andrews aliweza kuvuka kriketi 10, katika mechi yake ya hivi majuzi Jumapili aliweza 40. “Unapotoka nje ya uwanja, umeshinda vita,” anasema.
#KonceptTvUpdates