Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imetangaza bei mpya za mafuta zitakazoanza kutumika nchini kuanzia septemba 6,2023 ambapo taarifa hiyo iliyotolewa jana Jumanne Septemba 5, 2023 saa 4 usiku na Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Dk James Mwainyekule imeonesha kuwa kuanzia leo Jumatano Septemba 6 mwaka huu jijini Dar es Salaam Petroli itauzwa Sh3,213 na dizeli itauzwa kwa Sh3,259.
Bei hizo zinamaanisha kuwa katika Mkoa wa Dar es Salaam petroli imeongezeka kwa Sh14 kutoka Sh3,199 Agosti huku dizeli ikiongezeka zaidi kwa Sh324.
Hata hivyo kwa upande wa mikoa mingine yenye bandari zinazoshusha mafuta nchini pia bei ya mafuta imeongezeka; Mtwara kwa mwezi huu lita moja ya petrol itauzwa Sh3,285 ikiongezeka kutoka Sh3,271 na upande wa dizeli itauzwa Sh3,332 kutoka Sh3,008 mwezi uliopita.
Aidha, bei ya mafuta pia imepaa kwa mkoa wa Tanga ambapo kwa sasa lita moja ya petroli itauzwa Sh3,259 kutoka Sh3,245 Agosti huku dizeli nayo ikiongezeka zaidi kutoka Sh2,981 Agosti hadi Sh3,305.
Wakati hali ikiwa hivo katika mikoa mitatu yenye bandari, pia bei itaongezeka zaidi mkoani Kagera katika eneo la Kyerwa (Ruberwa) ambapo petroli itauzwa Sh3,450 kwa lita na dizeli itauzwa Sh3,497 kwa lita.
#KonceptTVUpdates