Mbunge wa Tarime Vijijini (CCM) Mwita Waitara amehoji ni lini serikali itaongeza posho za Madiwani na Wenyeviti wa Mitaa/Vijiji ili kuhimili gharama za maisha akitaja kuwa kwa miaka 8 akiwa Bungeni hakuwahi kusikia mpango wa serikali ama mjadala wa kuongeza posho hizo.
Waitara ambaye alikuwa Naibu Waziri ofisi ya Rais TAMISEMI amesema hii leo kuwa kuna haja ya serikali kufanya hivyo ili kuwawezesha viongozi hao kusimamia vyema miradi ya serikali inayotekelezwa katika maeneo yao.
Wabunge wengine waliouliza maswali ya nyongeza waliohoji kuhusiana na suala la posho za madiwani na wenyeviti wa CCM ni Festo Sanga (Makete), Rashid Shangazi (Mlalo) na Neema Lugangira (Viti Maalum).
Akijibu Naibu Waziri katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Festo Dudange amesema Serikali inatambua kazi kubwa inayofanywa na madiwani na wenyeviti wa vijiji katika kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi.
Amesema kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka za Serikali za Mitaa kila halmashauri inatakiwa kuweka utaratibu wa kuwalipa posho, madiwani na wenyeviti wa mitaa na vijiji kutoka katika vyanzo vya mapato ya ndani ya halmashauri.
“Kutokana na changamoto za mapato kwenye halmashauri nyingi nchini, Serikali ilianza kutenga bajeti katika mwaka wa fedha 2021/22 kwa ajili ya kulipa posho za waheshimiwa madiwani pamoja na wenyeviti wa vijiji,” amesema dkt Dudange.
aidha ameongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2023/24 Serikali imetenga kiasi cha Sh22.5 bilioni kwa ajili ya kulipa posho za madiwani na Wenyeviti wa vijiji katika halmashauri 168.
#KonceptTVUpdates