Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amefungua mkutano wa mwaka wa kiutendaji wa Maafisa Ustawi wa Jamii kutoka Wizara za Kisekta, Taasisi za umma pamoja na sekta binafsi zinazotoa huduma za Ustawi wa Jamii nchini na kutoa maelekezo mahsusi yatakayofanya sekta hiyo kuwa imara na kutoa huduma bora katika Taifa.
Dkt.Doto Biteko amefungua Mkutano huo jana Septemba 6, 2023 jijini Dodoma ambapo mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, Naibu Waziri, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Deogratius Ndejembi, na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Patrobas Katambi.
Akifungua Mkutano huo kwa niaba ya Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango, Dkt.Biteko ametoa maagizo mbalimbali kwa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Ofisi ya Rais TAMISEMI na wadau wengine ikiwemo ya kuhakikisha kuwa mchakato wa mapitio ya sheria ya mtoto na kanuni zake unakamilika ili kuhakikisha watoto wanapata ulinzi na malezi stahiki.
Amewaelekeza pia, wahakikishe mchakato wa sheria ya wataalamu wa ustawi wa jamii inakamilika ili kupanua wigo na kusimamia maadili ya utoaji wa huduma za ustawi wa jamii.
Aidha, Wakurugenzi wa Halmashauri wametakiwa kutenga fedha kwa ajili ya huduma za Ustawi wa Jamii kwa mujibu wa mwongozo wa mipango, bajeti na taarifa za Ustawi wa Jamii.
Vilevile, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma wametakiwa kuendelea kutoa ajira kwa maafisa Ustawi wa Jamii ili kusaidia kutoa huduma bora za Ustawi wa Jamii
Dkt. Biteko ameagiza pia kuimarishwa kwa programu ya huduma ya afya ya akili na msaada wa kisaikolojia ili kupunguza athari na changamoto zinazotokea ndani ya familia na jamii.
Agizo jingine lililotolewa ni uwekaji wa mfumo madhubuti wa ufuatiliaji wa makao ya Watoto na Makazi ya wazee ili kuhakikisha malengo ya msingi ya kuanzishwa vituo hivyo yanafuatwa kikamilifu na hayaanzishwi kiholela.
#KonceptTVUpdates