Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. John Jingu amewataka watumishi wa Wizara hiyo kuunganisha mawazo na nguvu zao ili kutatua kero za wananchi kwa kutoa huduma bora.
Dkt. Jingu ameyasema hayo jana Septemba 04, 2023 mara baada ya kuwasili katika Ofisi za Wizara ya Afya zilizopo katika Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma, na kupokelewa na Menejimenti na Watumishi wa Wizara wakiongozwa na aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe pamoja na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumanini Nagu.
“Serikali ipo kwa ajili ya kuwahudumia wananchi, sisi wote hapa tuna uwezo mbalimbali, nina uhakika tukiunganisha mawazo yetu pamoja tutajua namna gani tufanye ili tuweze kutatua kero za wananchi”, amesema Dkt. Jingu
Aidha, Dkt. Jingu amewataka watumishi wa Wizara ya Afya kuimarisha mahusiano mazuri kazini kwa kuthaminiana, kuheshimiana na kupendana ili kutekeleza majukumu vizuri na kumrahisishia yeye kufanya majukumu yake vizuri kama alivyoagiza na Rais Samia Suluhu Hassan.
“Tunapokuwa katika mazingira haya ya kazi, ili tuweze kufanya kazi zetu vizuri ni lazima tuwe na mahusiano mazuri kazini kwa kuthaminiana, kuheshimiana na kupendana, lakini pia ni maelekezo aliyoyatoa Rais Samia Suluhu Hassan, kuheshimiana kazini kwa ngazi zote,” amesema Dkt. Jingu
Amesema, eneo la kazi ndio familia namba moja kwa kuwa tunatumia muda wetu mwingi kuwa kazini kuliko katika familia zetu za nyumbani, Mke, Mume na watoto, hivyo ili tuweze kufanya kazi zetu vizuri lazima kuwe na mahusiano mazuri kazini.
“Hata Kama mnauwezo mkubwa wa kufanya kazi kiasi gani lakini kama hakuna upendo, mahusiano mazuri kazini kuheshimiana, basi hakuna kazi itakayofanyika ikawa nzuri sababu ya kutokuwa na umoja”, amesema Dkt. Jingu
Pia, Dkt. Jingu amewataka watumishi wa Wizara ya Afya hao kuwa na tabia ya kumsikiliza Rais Samia popote anapoongea kwakuwa inawezekana akatoa maagizo yanayoihusu Sekta ya Afya, na kuanza kuyatekeleza kwa haraka.
#KonceptTVUpdates