Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameihimiza jumuiya ya kimataifa kusaidia kuifanya Afrika kuwa nguvu ya nishati jadidifu wakati wa mkutano wa kilele wa tabianchi unaolenga kuvutia uwekezaji wa kimazingira Afrika.
Mkutano huo wa siku tatu wa kilele ulioanza siku ya Jumatatu septemba 04,2023 Nairobi nchini Kenya, umewashirikisha wakuu wa nchi, serikali na viwanda, wakiwemo viongozi kutoka Msumbiji na Tanzania, pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen na mjumbe maalumu wa serikali ya Marekani anaeshughulikia Mabadiliko ya Tabianchi John Kerry.
Akizungumza kwenye Mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Gutgerres amesema nishati mbadala inaweza kuwa muujiza wa Afrika, lakini akaongeza kuwa sisi ndiyo tunapaswa kulifanya hilo litokee.
Huku dunia ikiwa imepungukiwa sana katika utekelezaji wa malengo yake ya kupunguza ongezeko la joto, Guterres amezungumza moja kwa moja na viongozi wa kundi la mataifa 20 yaliostawi na yanayoinukia kiuchumi duniani, G20, wanaokutana nchini India mwishoni mwa juma hili, na kuwataka kuchukuwa majukumu yao katika mapambano ya kupunguza joto la dunia.
“Leo nimerudia wito wangu kwa ulimwengu kuharakisha hatua za hali ya hewa ili kuepusha athari mbaya zaidi za mabadiliko ya tabianchi, kutimiza ahadi za kimataifa za kutoa msaada muhimu na kusaidia Afrika kufanya mabadiliko ya haki na ya usawa kwa nishati mbadala,” alisema Katibu Mkuu Guterres.
Hii leo mkutano huo umeshuhudia ahadi yake muhimu zaidi kufikia sasa, ambapo Umoja wa Falme za kiarabu umetowa dola bilioni 4.5 za kupambana na uchafuzi wa mazingira. Umoja wa Falme za Kiarabu UAE, pia utakuwa mwenyeji wa mkutano wa kilele wa COP28 mjini Dubai mwezi Novemba hadi Desemba.
Sultan Al Jaber, ambaye anaongoza kampuni ya kitaifa ya mafuta ya UAE ADNOC na kampuni ya nishati mbadala inayomilikiwa na serikali ya Masdar, amesema uwekezaji huo utaanzisha miradi kadhaa muhimu ya nishati safi barani Afrika.
#KonceptTVUpdates