Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde ameainisha vipaumbele vyake katika Sekta ya Madini ili kuhakikisha taifa linanufaika na uwepo wa Madini yanayopatikana hapa nchini.
Ameainisha hayo septemba 11 , 2023 wakati akizungumza katika Mkutano wa Wachimbaji Wadogo wa Madini kutoka Shirikisho la Wachimbaji wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA) uliofanyika jijini Dodoma.
Akizungumzia juu ya kuongeza taarifa za utafiti wa jiolojia Mavunde amesema kuwa moja ya vipaumbele vyake katika sekta ya madini ni kuijengea uwezo Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) ili iweze kufanya utafiti wa kina kwa ndege yaani (Air Born Geophysical Survey) utakaotoa taarifa na kuonesha utajiri wa madini yaliyopo nchini kwa kiwango kikubwa tofauti na sasa ambapo ni asilimia 16 tu ya eneo lote nchi nzima limefanyiwa utafiti wa kina.
Waziri Mavunde ameongeza kuwa GST inapaswa kufanana na taasisi nyingine za Utafiti wa Madini duniani ikiwa na maabara ya kisasa itakayotumiwa na wachimbaji wote nchini.
“Ndugu zangu tukipiga picha ya miamba yote nchi nzima, tutapata taarifa sahihi ya kijiolojia ili wachimbaji wasifanye kazi zao kwa kubahatisha , uchimbaji ni Sayansi sio bahati wala uchawi, mchimbaji mwenye taarifa ya utafiiti wa kijiolojia atafanikiwa zaidi kupitia Sekta hii ya Madini” amesema Mavunde.
Akielezea faida za utafiti huo Mavunde amesema taarifa za kina kwa jiolojia utaleta tija na mapinduzi makubwa katika sekta nyingine akitolea mfano sekta ya kilimo hasa katika utafiti wa udongo, mbolea na sekta ya maji katika uchimbaji visima.
Aidha, ametaja mpango mwingine kuwa Wizara itaenda kuwa na makumbusho ya madini ili wananchi wapate kuona na kufahamu madini yanayopatikana nchini kuliko kuyasikia tu.
#KonceptTVUpdates