Tangu kuondoka kwa Uhispania, iliyoitawala nchi hiyo katika enzi za ukoloni mnamo miaka ya 1976, eneo hilo linadhibitiwa 80% na Morocco wakati kundi la Polisario Front linaendelea kuomba uhuru wa eneo hilo.
Kwa muda mrefu Sahara Magharibi ilikuwa koloni ya Uhispania. Mnamo mwaka 1975, makubaliano yaliyotiliwa saini mjini Madrid yalimaliza utawala huo wa ukoloni na kugawanya eneo hilo mara mbili. Eneo la kusini mwa Sahara Magharibi lilipewa Mauritania, ambayo ilirejesha sehemu hiyo miaka sita baadaye, wakati eneo la kaskazini na katikati lilichukuliwa na Morocco.
Jiografia ya nchi hizi
Morocco ni nchi inayopatikana kwenye pembe ya kaskazini-Magharibi mwa Afrika na upande wa Kusini imepakana na Sahara Magharibi na upande wa mashariki imepakana na Algeria, huku upande wa Magharibi ikipakana na bahari ya Atlantiki.
Jiografia ya Morocco inajumuisha safu zisizopungua nne za milima, pamoja na mabonde ya mito, pwani nzuri za mchanga, na maeneo mapana ya jangwa.
Jamhuri ya Waarabu ya Kidemokrasia ya Sahara (Sahrawi Arab Democratic Republic, SADR) ama Sahara Magharibi ni eneo lililo kaskazini-magharibi mwa Afrika, likiwa kusini mwa Morocco na upande wa mashariki imepakana na Mauritania na Magharibi imepakana na bahari ya Atlantiki. Uwepo wake katika kingo za Bahari ya Atlantiki unaipa umuhimu wa kimkakati kwa mataifa ya Ulaya na Afrika kaskazini.
Historia ya nchi hizi enzi za Ukoloni
Uwepo wa Morocco katika eneo lililo lango linalozikutanisha bahari ya Mediterranea na Bahari ya Atlantiki liliyavutia madola ya Ulaya kutaka kuitawala.
Mnamo 1912 baada ya kusainiwa kwa Mkataba wa Fez, Morocco ilitangazwa kuwa chini ya ulinzi wa Ufaransa (Protectorate), mwaka huo huo baada ya makubaliano kati ya Ufaransa na Uhispania Sahara Magharibi ikatangazwa kuwa chini ya ulinzi wa Uhispania (Protectorate) na ikaitwa ‘Spanish Sahara’ ama Sahara ya Uhispania.
Uhispania ilivutiwa na uwepo wa Sahara katika kingo za bahari ya Atlantiki iliyowapa waHispania eneo kubwa zaidi kwa ajili ya uvuvi. Hivyo Sahara ikatawaliwa na Uhispania huku Morocco ikitawaliwa na Ufaransa.
Ukoloni katika nchi ya Morocco ulifika ukomo Mnamo Machi 1956 ambapo Morocco ilijipatia Uhuru wake toka kwa Ufaransa baada ya machafuko na hisia kali za utaifa (nationalism).
Katika Vyuo Vikuu vya Morocco wanafunzi wenye asili ya Sahrawi pamoja na wenzao waliokuwa nchini Algeria na Mauritania waliunda kile kilichokuja kuitwa ‘The Embryonic Movement for the Liberation of Saguia el-Hamra na Rio de Oro’ kwa lengo la kuikomboa Sahara ambayo bado ilikuwa chini ya utawala wa kikoloni wa Uhispania.
Mnamo Mei 1973 vuguvugu lililopewa jina la Polisario Front liliundwa ambalo lilijumuisha hasa watu wenye asili ya Sahrawi toka Morocco, Algeria na Mauritania huku lengo kuu likiwa ni kuikomboa Sahara Magharibi (SADR) kwa gharama yoyote ile.
Vuguvugu hilo lilipata kuungwa mkono na Algeria na Libya na Mauritania.
Mwanzo wa uadui
Wakati Uhispania ikijiandaa kuondoka Sahara Magharibi, Novemba Mwaka 1975 Morocco ilituma raia 350,000 waliovuka mpaka na kuingia Sahara katika kile kinachojulikana kama maandamano ya ‘Green march’ kwa lengo la kuishinikiza Uhispania kuikabidhi Morocco koloni hilo. Makubaliano yalitiliwa saini siku chache baada ya maandamano ya amani yaliyoandaliwa na Mfalme Hassan II wakati zaidi ya raia 350,000 wa Morocco walizuru eneo hilo. Tangu wakati huo, hali ya mvutano iliibuka kati ya utawala wa Hassan II na kundi la waasi la Polisario Front.
Uhispania haikuweza kukabiliana na vuguvugu hilo hivyo ikalazimika kutafuta suluhu kwa njia ya amani na siku chache baadaye ndani ya mwezi huohuo mwaka 1975 nchi za Morocco, Mauritania na Uhispania zilisaini Mkataba wa Madrid, katika mkataba huu Uhispania ilizikabidhi Mauritania na Morocco eneo la Sahara Magharibi kwa sharti la kuwa Uhispania itachukua 35% za migodi yote ya Fosfeti (Phosphate) iliyopo Sahara Magharibi na haki za uvuvi ( Fishing rights) katika maji ya Sahara Magharibi kwa muda wa miaka kumi.
Algeria haikukubaliana kabisa na suluhu hilo kwakuwa iliona kuwa watu wa Sahara Magharibi waliowakilishwa na Polisario Front hawakushirikishwa wakati wa majadiliano hayo na ikatishia kupigana dhidi ya Morocco kuitetea Sahara Magharibi.
Toka mwaka huo Polisario Front walipewa hifadhi nchini Algeria pia walipewa vituo vya kijeshi, misaada ya silaha na uungwaji mkono wa kisiasa. Polisario Front ilianzisha mashambulizi ya kupigana na Mauritania na Morocco ili kuwa nchi huru.
Kwa kuanza tu, ilipotimu Februari 27, 1976 Polisario Front ilitangaza kuwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Sahrawi kuwa ni nchi huru na mipaka yake ni eneo lote la Sahara Magharibi.
Awali Jamhuri hiyo ilitambuliwa na idadi ndogo ya nchi, mojawapo ikiwa ni Algeria.
Mapigano yalipamba moto baina ya Polisario Front ikiungwa mkono na Algeria dhidi ya Mauritania na Morocco ambazo ziliiona Polisario Front kama kikundi cha waasi.
Mwaka 1979 Mauritania ilitupilia mbali madai yake kuwa eneo la Sahara Magharibi ni lake kwa mujibu wa mkataba wa Madrid hivyo Morocco ikabaki peke yake kuendelea na madai hayo na ilifanikiwa kutwaa sehemu kubwa ya eneo la Sahara Magharibi.
Mapigano kati ya Polisario Front na vikosi vya Morocco yaliendelea hadi 1991 wakati ambao Umoja wa Mataifa uliishinikiza kusitishwa kwa mapigano, wakati huo Polisario Front ilidhibiti 20% tu ya eneo lote inalodai kuwa ni la kwake.
Mnamo mwaka 1976, Polisario Front ilitangaza eneo hilo kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Sahrawi (SADR). Mwaka 1984, ilijiunga na Umoja wa Afrika (ambayo ilikuwa bado ikiitwa OAU) na OAU iliitambua nchi ya Sahara Magharibi na kuipa uanachama wa Umoja wa Afrika, Morocco iligomea uamuzi huo kwa kuamua kujitoa kwenye umoja huo wa OAU.
Mgogoro huu umekuwa ukiendelea mpaka hivi karibuni kati ya Polisario Front na majeshi ya kifalme ya Morocco kitu ambacho kinatishia maisha ya watu wanaoishi katika eneo hilo na kuchochea mgawanyiko zaidi katika Umoja wa Afrika.
#KonceptTVUpdates