Msemaji wa Jeshi la Polisi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP David Misime amesema leo Septemba 19, 2023 Jijini Dodoma kuwa Jeshi la Polisi na Waandishi wa habari ni wadau muhimu katika kufanya kazi zao za kila siku wakati akifungua Mdahalo wa kitaifa kuhusu ulinzi na Usalama kwa Waandishi wa Habari uliowashirikisha wadau mbalimbali wa Habari na Jeshi la Polisi.
SACP Misime alisema kazi zinazofanywa na Waandishi wa habari na Jeshi la Polisi lengo lake ni kuisaidia nchi ya Tanzania katika nyanja mbalimbali ikiwemo kukuza uchumi na kuwafanya Watanzania waishi kwa amani na utulivu bila ya kufanyiwa uhalifu.
Alisema mdahalo huo umefanyika katika kipindi muafaka ambapo amewataka washiriki kufanya mdahalo wenye afya ya kujenga taswira nzuri ya Tanzania na kuzingatia maslahi mapana ya Tanzania.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) Kenneth Simbaya amesema lengo la mdahalo huo ni kuimarisha uhusiano ulipo baina ya Jeshi la Polisi na Waandishi wa Habari ili kuwafanya Waandishi wa habari kufanya kazi bila hofu.
Simbaya amesema Waandishi wa habari wanapaswa kufanya kazi zao bila hofu ili kukuza uhuru wa kujieleza na kuimarisha demokrasia nchini.
#KonceptTVUpdates