Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kufanya mabadiliko makubwa katika sheria ya utumishi ili kuwapa kipaumbele wale wote wanaojitolea katika taasisi mbalimbali za umma. Hatua hii inalenga kuongeza fursa za ajira kwa wanaojitolea na kuthamini mchango wao kwa jamii na nchi kwa ujumla.
Naibu Waziri wa Utumishi na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, alitoa taarifa hii Jumatatu, Septemba 4, 2023, Bungeni Jijini Dodoma. Alipokuwa akijibu maswali ya wabunge, alieleza kuwa serikali imeanza mapitio ya sheria mbalimbali zinazohusiana na utumishi wa umma, ikiwa ni pamoja na Sura no. 298 ya sheria ya utumishi wa umma, sera ya Menejimenti ya ajira ya umma toleo la pili la 2008, kanuni ya utumishi wa umma ya 2022, na miongozo inayohusu masuala ya ajira.
Kikwete alisema kuwa suala la kujitolea limekuwa na miongozo mingi, na kwa hivyo, serikali inafanya marekebisho ili kuweka kigezo cha kujitolea katika sheria ya utumishi wa umma. Mara baada ya marekebisho kukamilika, muswada wa sheria hiyo utawasilishwa Bungeni kwa ajili ya kujadiliwa na wabunge, na hatimaye kuwa sheria.
Hatua hii itawawezesha wanaojitolea kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya nchi na kuona thamani ya jitihada zao zinathaminiwa na serikali. Pia, itasaidia kujenga jamii inayothamini kujitolea na kuchochea roho ya kujitolea kwa vijana na watu wengine katika jamii.
#KonceptTvUpdates