Timu ya soka ya Tanzania ‘Taifa Stars’ wameibuka mashujaa wa taifa kwa kufuzu Michuano ya Mataifa Afrika kwa mara ya tatu, ‘AFCON 2023’ wakiwa ugenini dhidi ya Algeria, katika dimba la May 19, 1956 nchini Algeria.
Matokeo ya bila kufungana ndani ya dakika 90 yameifanya Stars kumaliza nafasi ya pili katika kundi F, kwa alama 8 nyuma ya Algeria vinara wa kundi wenye alama 16 hivyo timu mbili za juu zimekata tiketi ya kushiriki AFCON itakayovurumishwa huko Ivory Coast.
Uganda ‘The Cranes’ licha ya kupata ushindi wakiwa ugenini wa goli mbili kwa sifuri dhidi ya Niger wamemaliza nafasi ya tatu wakiwa na alama 7 na mkiani yupo Niger kwa alama 2. Hii inakuwa mara ya tatu kwa Stars kufuzu kucheza fainali hizo, ikianza 1980, 2019 na sasa 2023.
Kama ilivyo ada, ‘chanda chema huvikwa pete,’ Rais Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za pongezi kupitia Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo, Saidi Yakubu aliyepo katika msafara wa Stars huko Algeria.
#KonceptTVUpdates