Tanzania kupitia Wizara ya Afya imeendeleza jitihada za kuboresha upatikanaji wa dawa nchini Botswana kwa kutoa ombi la ushirikiano. Waziri wa Afya wa Tanzania, Ummy Mwalimu, alifanya ziara nchini Botswana siku ya Agosti 31, 2023, na kufanya mazungumzo muhimu na Waziri wa Afya wa Botswana, Dkt. Edwin Dikolot, kuhusu masuala ya upatikanaji wa dawa nchini Botswana.
Katika ziara hiyo, Waziri Ummy Mwalimu alisema, “Nimewasilisha ombi kwa Waziri wa Afya wa Botswana, Mhe. Dkt. Edwin Dikolot, la kutaka Tanzania iweze kuisaidia nchi hii katika kuimarisha upatikanaji wa dawa. Tanzania ina uzoefu wa kutosha katika ununuzi wa dawa ambapo imeingia mikataba na wazalishaji wakubwa wa dawa duniani wapatao 233.”
Ni jambo la kujivunia kwamba kupitia mfumo wake wa ununuzi wa dawa, Tanzania inaweza kununua aina za dawa tofauti 2209. Pia, Tanzania imepewa jukumu la ununuzi wa dawa kwa pamoja na nchi nyingine mbili, Comoro na Seychelles. Mpango huu wa ununuzi wa pamoja umefanikisha kupunguza gharama ya ununuzi wa dawa kwa asilimia 53, kwa kuzingatia azimio la Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), ambalo linahimiza Bohari ya Dawa ya Tanzania kusaidia nchi wanachama katika upatikanaji wa dawa.
Waziri wa Afya wa Botswana, Dkt. Edwin Dikolot, alimshukuru Waziri wa Afya wa Tanzania, Ummy Mwalimu, kwa kuleta wazo hili la ushirikiano katika sekta ya afya. Alielekeza Taasisi ya Dawa ya Botswana kuanza mazungumzo na Bohari Kuu ya Dawa ya Tanzania ili kuchunguza fursa za ushirikiano na kuimarisha upatikanaji wa dawa nchini Botswana.
Ushirikiano huu unaweza kuwa ha tua muhimu katika kuboresha huduma za afya nchini Botswana, na pia kuonyesha umuhimu wa nchi za Afrika kusaidiana katika masuala ya afya ili kuhakikisha kuwa dawa zinapatikana kwa wananchi kwa bei nafuu zaidi.
#KonceptTvUpdates