Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga ameweka historia kwa kuwasha umeme kwa mara ya kwanza katika Kijiji cha Ikindwa (Bukene) Wilayani Nzega mkoani Tabora, tangu kuanzishwa kwa kijiji hicho baada ya nchi kupata uhuru.
Kapinga amefanya tukio hilo, tarehe 25 Septemba 2023 katika Wilaya ya Nzega mkoani Tabora alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya Mradi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini mzunguko wa tatu Awamu ya Pili katika wilaya hiyo kwa kuwasha umeme katika kijiji husika na kuzungumza na wananchi wa eneo hilo.
Akizungumzia mradi huo, Kapinga amesema Serikali imetenga fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza mradi wa usambazaji umeme vijijini katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo vituo vya afya, Taasisi za elimu, Taasisi za Dini, Masoko, Visima vya Maji na Mashamba.
“Niwatoe hofu kuwa wananchi wote mtamfikiwa na umeme, kazi iliyombele yenu ni kusuka waya katika nyumba zenu, ili umeme utakapofika maeneo yenu kazi iwe ni kuwaunganisha tuu tena kwa gharama nafuu ya shilingi 27,000. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan ameshatoa maelekezo kuwa wananchi wote waunganishiwe umeme” alisema Kapinga.
Aidha ametoa siku saba kwa mkandarasi anaetekeleza mradi huo katika kijiji cha Ikindwa kuwalipa ujira wao vijana waliofanya kazi ya kuchimba mashimo, kusimika nguzo pamoja na kuvuta nyaya ambapo mpaka sasa bado hawajalipwa fedha zao.
Alimueleza mkandarasi huyo kuwa jukumu la kusimamia malipo ya wafanyakazi hao ni la kwake na si la Wakala wa Nishati Vijijini (REA) hata kama anaweka kampuni za kumsaidia katika kazi hiyo.
Sambamba na hilo aliwataka wakandarasi wote kukamilisha na kukabidhi kazi waliyopewa ya kusambaza umeme vijijini ifikapo mwisho wa mwezi Desemba 2023 tena bila visingizo vya aina yeyote ili kumaliza kazi ya kusambaza umeme vijijini na kuhamia katika Vitongoji.
#KonceptTVUpdates