Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amemuagiza Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt Dotto Biteko kuendelea na jitihada za kupata ufumbuzi wa changamoto ya tatizo la mafuta nchini huku akitaka jambo hilo lifanyike ndani ya wiki moja.
Waziri Majaliwa ameyasema hayo na kutoa agizo hilo mapema hii leo septemba 7,2023 bungeni jijini Dodoma mara baada kuulizwa swali na mbunge wa Mlalo, Rashid Shangazi wakati wa maswali kwa Waziri mkuu.
Mbunge huyo alihoji mkakati wa serikali kutokana na sintofahamu ya upatikanaji wa mafuta katika vituo mbalimbali vya kuuza nishati hiyo hivi karibuni, ambapo mafuta ya petrol na diesel yamekuwa hayapatikani katika baadhi ya maeneo, lakini bei ikishatangazwa yananza kupatikana, lakini pia alizungumzia suala la bei ya mafuta kubadiika mara kwa mara.
Akijibu swali hilo Waziri Mkuu amesema ni kweli kuna changamoto ya upatikanaji mafuta nchini, ambapo baadhi ya vituo maeneo kadhaa vilikuwa havina mafuta na kwamba serikali inafanya jitihada mbalimbali kutatua tatizo hilo kuanzia Wizara ya Nishati na hata Kamati ya Bunge ya Nishati wamekaa mara kadhaa kwa ajili ya jambo hilo.
“Nikiri kwamba tuna changamoto ya upatikanaji wa mafuta nchini kwasababu kuna vituo vinakosa mafuta, zipo jitihada zinafanywa na Serikali ikiwemo wizara husika…. Tumeanza kumuona Naibu Waziri Mkuu (Dkt Biteko) akifanya kazi kadhaa kwakuwa ameshaanza hii Kazi niendelee kumuagiza aendelee na hili, muhimu nishati hii ipatikane nchini,” amesema Majaliwa.
#KonceptTVUpdates