Mwakilishi wa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Prisius Mwanda amewataka Wakuu wa Upelelezi wa Mikoa , Wakuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa wa Mikoa, Wakuu wa Upelelezi wa Mikoa, na Waendesha Mashtaka wa Mikoa kuhakikisha wanalinda mifumo ya kifedha Iliyopo kwa kufanya uchunguzi madhubuti kwa kukamata mali zinazotokana na uhalifu kwa kuwa wahalifu wengi hutumia udhaifu wa mifumo kutimiza adhma yao.
Wito huo umetolewa Oktoba 1, 2023 wakati akifunga Kikao cha Menejimenti ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kilichofanyika kwa muda wa siku tatu Jijini Dodoma.
Mwanda amesema kuwa uhalifu ni suala mtambuka na mbinu zake hubadilika kulingana na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia na kimsingi uhalifu hauna mipaka hivyo taasisi zote zinazohusika Kupambana na uhalifu ni lazima zijidhatiti katika kutumia taarifa kwa lengo la kubaini miamala inayotokana na Mali zitokanazo na uhalifu na hatimaye kuzitaifisha pale zinapobainika.
Ameongeza kuwa ili taasisi hizo ziweze kupata matokeo makubwa katika mapambano ya uhalifu hawana budi kuongeza ushirikiano wa taasisi za ndani na nje ya nchi yetu, kutumia mbinu za kisasa pamoja na Teknolojia.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Silvester Mwakitalu alisema kuwa washiriki wa kikao hicho waliweza kupata mafunzo ya kuwajengea uwezo kiutendaji katika kufanikisha uhalifu unadhibitiwa hapa nchini.
DPP Mwakitalu alitaja mafunzo waliyoyapata ni pamoja na namna ya kuthibitisha makosa ya mtandao Mahakamani, uhalifu wa utakatishaji wa fedha haramu, upelelezi wa makosa ya Mali zinazotokana na uhalifu, utaifishaji wa Mali zinazotokana na uhalifu pamoja na uhalifu unaovuka mipaka.
#KonceptTVUpdates